HOJA
BINAFSI YA KABWE ZUBERI ZITTO (MB) KUHUSU KULITAKA BUNGE KUCHUNGUZA NA
KUIELEKEZA SERIKALI KUCHUKUA HATUA DHIDI YA RAIA WA TANZANIA WALIOFICHA
FEDHA NA MALI HARAMU NJE YA NCHI
Mbunge wa Kigoma Kaskazini, Zitto Kabwe.
[Chini ya Kanuni ya 54(1) na (2)]
UTANGULIZI:
Mheshimiwa Spika,
Mnamo
tarehe 2 Novemba 2012 niliwasilisha barua ya kusudio la kuwasilisha
Bungeni Hoja binafsi kuhusu suala hilo hapo juu. Lengo la Hoja binafsi
hiyo ni kuitaka Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, kuwasiliana
na Taasisi ya Benki ya Dunia kupitia kitengo cha ‘Assets Recovery’
kurejesha fedha haramu zilizofichwa na Raia wa Tanzania katika mabenki
huko nchini Switzerland. Ofisi yako ilinitaka nilete maelezo ya ziada
kuhusu hoja hiyo ili ipatiwe nafasi ya kupangwa kwenye ratiba za
Bunge. Baada ya kuleta maelezo hayo Ofisi yako imenipa nafasi
kuwasilisha hoja hii mbele ya Bunge lako tukufu. Kwa heshima na taadhima
ninawasilisha mbele ya Bunge lako tukufu hoja hii muhimu sana katika
kuhakikisha kwamba Taifa letu linaziba mianya ya ufisadi na hususani
utoroshwaji wa fedha za kigeni za Tanzania.
Mheshimiwa Spika,
Mwezi
Juni mwaka 2012, Benki Kuu ya Switzerland (National Bank of
Switzerland) ilitoa taarifa kwa umma kuhusu raia wa mataifa mbalimbali
duniani wenye dhamana kwenye mabenki nchini humo. Benki hiyo ilitangaza
kwamba Jumla ya dola za Kimarekani milioni 196 (milioni mia moja tisini
na sita) zilikuwa zimehifadhiwa kwenye akaunti za mabenki mbalimbali
nchini humo na kwamba wenye fedha hizo ni Raia wa Tanzania. Fedha hizo
ni zaidi ya shilingi bilioni 314 (mia tatu kumi nanne bilioni)
ukizibadilisha kwa thamani ya fedha za Tanzania.
Mheshimiwa Spika,
Mazungumzo
yangu ya mwisho niliyoyafanya jana usiku na wachunguzi waangu binafsi
yameongeza taarifa ya ziada muhimu. Kwanza, kiwango cha fedha kinacho
milikiwa na watanzania nchini Switzerland peke yake ni takribani mara 20
ya kiwango kilicho tangazwa na Benki ya Tanifa ya nchi hiyo. Kwa mfano,
Benki ya UBS peke yake ina maofisa 240 wanaohusika na Tanzania peke
yake. Kila ofisa mmoja husimamia mteja mwenye kiwango kisicho pungua
dola za marekani milioni 10.
Fedha
hizi ni sehemu tu ya fedha ambazo watanzania wanazificha katika mabenki
mbalimbali ya nje ya nchi, na ndani ya hesabu hizi hamna fedha zilizo
nchi nyingine,kama visiwa Jersey, Mauritius na Cayman Islands maana nchi
nyingine hazina utaratibu huu wa kuweka wazi kama ilivyo kwa nchi ya
Swistzerland kwa mwaka huu.
Mheshimiwa Spika,
Gazeti
la The Guardian On Sunday la tarehe 23 Juni 2012 lilimnukuu Mkurugenzi
Mkuu wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa ndugu Edward Hosea
akisema kwamba siku ya jumatatu tarehe 24 Juni mwaka 2012 angeandika
Barua kwenda Mamlaka za Switzerland kutaka kupewa orodha ya majina ya
raia wa Tanzania wenye fedha katika akaunti zilizotajwa. Hata hivyo
mpaka ninaleta maelezo haya umma wa Watanzania haujalezwa kama barua
hiyo iliandikwa na majibu yake yalikuwa ni nini. TAKUKURU ndio mamlaka
pekee hapa nchini ambayo inaweza kupata orodha ya majina ya watu wenye
mabilioni haya kwa njia za halali na hasa kwa watu ambao ni ‘Politically
Exposed Persons’kama Wabunge na waliowahi kuwa wabunge, Mawaziri na
waliowahi kuwa Mawaziri na viongozi wengine wa ngazi za juu katika Taifa
letu.
Mheshimiwa spika,
Nchi
nyingine duniani zimetumia njia mbali mbali kuhakikisha fedha haramu
zinazo toroshwaa zinarejea nchini kwao. Marekani na Ujerumani wao
waliamua kununua CDs kutoka kwa waliokua wafanyakazi wa mabenki ya
Switzerland, wakagundua Raia wao walioficha fedha nje na kuwatoza kodi
kutokana na fedha hizo. Ujerumani wao wameingia mkataba wa kupashana
taarifa za kikodi na nchi ya Switzerland ili kuwatoza kidi raia wao
wenye fedha huko. Hata hivo mkataba huu wa kikodi haujapitishwa na Bunge
la Ujerumani Bundesrat kwani chama kikuu cha upinzani cha SPD
kinapinga, na tayari chama hicho kimenunua CDs zenye majina ya Raia wa
Ujerumani wenye akiba nje.
Hivi
karibuni gazeti moja nchini Ugiriki limechapisha orodha ya wagiriki
walioficha fedha zaio huko Switzerland. Orodha hii inatokana na orodha
ambayo alie kua Waziri wa Fedha wa Ufaransa Christine Lagarde aliipa
serikali ya Ugiriki, lakini serikali hiyo haikuifanyia kazi.
Mheshimiwa Spika,
Kiufupi,
toka taarifa za Benki ya Taifa ya Switzerland kutangazwa, Serikali
haijachukua hatua yeyote ya maana kuhakikisha kuwa suala hili
linafanyiwa uchunguzi wa kina na hatua stahili dhidi ya watoroshaji wa
fedha hizo zinachukuliwa ikiwemo kurejeshwa kwa fedha hizo nchini kwa
ajili ya maendeleo ya Taifa letu. Ikumbukwe kwamba katika watanzania
wenye fedha huko nje wapo ambao fedha zao wamezipata kihalali kutokana
na shughuli za kibiashara na wapo ambao wamepata fedha hizi kwa njia za
rushwa. Uchunguzi wa kina ni muhimu sana ili kuweza kutofautisha kati ya
Fedha haramu na fedha halali. Vilevile uchunguzi unatakiwa kutofautisha
katika watu wenye fedha halali kama walifuata taratibu za kisheria za
nchi zinazoruhusu raia wa Tanzania wanaoishi Tanzania kuwa na akiba ya
fedha za kigeni nje ya Tanzania. Kitendo cha Serikali kukaa kimya bila
kuchukua hatua kinaashiria ama kutotimiza wajibu au kwamba wanaopaswa
kuchukua hatua ni washirika wa utoroshaji huu wa fedha za nchi na
kuzificha katika mabenki ya nje.
Mheshimiwa Spika,
Kabla
ya kueleza kwa kina vyanzo viwili vikubwa vya fedha kwa raia wa
Tanzania wanaomiliki fedha na mali katika mabenki nje ya nchi
nieleze kwamba, Watu hufungua akaunti nje ya nchi au kumiliki mali nje
ya nchi kwa sababu kuu mbili. Moja ni kuficha fedha haramu
zilizopatikana kwa njia zisizo halali na mbili kukwepa kodi kutokana na
mapato yao. Njia ya kwanza hutumiwa zaidi na wanasiasa na watendaji wa
Serikali (Politically exposed Personalities – PEPs) na njia ya pili
hutumiwa na wafanyabiashara wakubwa na hasa wafanyabiashara wanaouza
bidhaa nje ya nchi. Harakati zozote za kuchukua hatua dhidi ya makundi
haya yana faida ya kuzuia ufisadi kwa kuonyesha kwamba hakuna pa
kujificha iwapo ukifanya ubadhirifu , na kuongeza mapato ya Serikali kwa
kuhakikisha Raia wote wakazi wanalipa kodi inavyostahili.
Uchunguzi wa chanzo cha Fedha.
Mheshimiwa Spika,
Kwa
mujibu wa Taarifa ya Global Financial Integrity (GFI) ya mwaka 2008,
jumla ya dola za kimarekani bilioni 8 (dola bilioni nane) zimetoroshwa
kutoka Tanzania kati ya mwaka 1970 mpaka 2008. Kwa bei ya sasa ya dola
za kimarekani fedha hizi ni sawa na shilingi trilioni 13 (trilioni kumi
na tatu). Mpaka Mwezi Julai mwaka 2012 Deni la Taifa kuanzia mwaka 1961
lilikuwa ni dola za kimarekani bilioni kumi. Hii maana yake ni kwamba
fedha zote zilizotoroshwa kutoka Tanzania katika kipindi cha miaka 38
kingeweza kulipia asilimia themanini ya Deni la Taifa. Mwaka 2012/2013
Bunge limeidhinisha jumla ya shilingi trilioni 1.9 kulipia Deni la
Taifa.Suala hili ni changamoto kwa nchi mbalimbali za kiafrika ambapo
mabilioni yafedha hutoroshwa kila mwaka na watawala wala rushwa na
wafanyabiashara wasio waaminifu kwenda nje ya Afrika na kuliacha bara la
Afrika likiwa na ufukara wa kutupwa.
Mheshimiwa Spika,
Sehemu
ya Fedha hizi zilizotoroshwa zilitokana na ufisadi, nyingine zilitokana
na ukwepaji wa kodi na nyingine zilitokana na madeni ambayo Serikali
iliingia ambapo sehemu kubwa ya Madeni ilibaki huko huko ughaibuni
lakini bado Watanzania wanalipa madeni hayo. Hata hivyo Fedha
zilizotokana kutokana Ufisadi na zile za ukwepaji kodi ni nyingi zaidi
katika fedha zilizotoroshwa kutoka Tanzania.
Mheshimiwa Spika,
Kwa
mfano kati ya mwaka 2003 - 2005 Tanzania iligubikwa na ufisadi mkubwa
sana wa Fedha kutoka Benki ya Tanzania ambapo jumla ya shilingi bilioni
155 zililipwa kutoka Benki Kuu ya Tanzania kwenda Benki ya NedBank ya
Afrika Kusini kama malipo ya mkopo ambao Serikali iliudhamini kwa ajili
ya mradi wa uchimbaji dhahabu wa meremeta. Fedha hizi zilikuwa ni mara
kumi na tano ya mkopo uliodhaminiwa na Serikali. Uchunguzi wetu
unaonesha kuwa asilimia 70 ya fedha za mradi wa meremeta ziliishia
kwenye Benki nchini Switzerland kupitia nchi ya Mauritius.
Mheshimiwa Spika,
Kampuni
ya Meremeta ambayo baadaye ilibadilishwa jina na kuitwa TanGold
ilianzishwa kama mradi wa kutorosha mabilioni ya fedha za nchi kwenda
kwa uhusika mkubwa sana wa Serikali. Nawasilisha mezani kwako barua
kutoka Ofisi ya Rais Ikulu ya tarehe 20 Agosti 2001, yenye kumbukumbu
nambari SHC/M.100/4/A kwenda Benki ya Deutsche Bank tawi la Uingereza
kuitambulisha Kampuni ya Meremeta na Kampuni ya Nedcor Trade Services
Limited ya Afrika ya Kusini ili ipewe mkopo. Barua hiyo inatambulisha
miradi miwili ya dhahabu (mgodi wa Tembo na Mgodi wa Buhemba) kwamba ni
miradi ya Wizara ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa. Baada ya barua hii
yaliyotokea ni mtandao mpana wa kuiba fedha za Tanzania kwenda Afrika
Kusini, baadaye Mauritius na kisha kuishia kwenye akaunti za watu
binafsi nchini Switzerland na visiwa vingine vya ukwepaji kodi (tax
havens). Kufuatilia barua hii kutoka Ikulu, mkopo wa dola za kimarekani
milioni kumi zilipatikana. Hata hivyo Serikali ya Tanzania kupitia Benki
Kuu ya Tanzania iliilipa Benki ya NedBank jumla ya dola za Kimarekani
138 milioni, dola milioni kumi kati ya hizi zililipwa kupitia kampuni ya
Deep Green Finance.
Mheshimiwa Spika,
Nilifanya
uchunguzi binafsi kuhusu suala hili. Nilijaribu kuwasiliana na Benki ya
NedBank ili kuweza kupata uhakika wa watu waliofaidika na uchotaji huu
mkubwa na wa kihistoria wa fedha za umma. Ufuatiliaji huu umeendelea vya
kutosha ila haujafika mwisho Hata hivyo taarifa nilizokusanya hadi
sasazimeonyesha hatari kubwa namna ambavyo watanzania wenzetu wenye
mamlaka wanavyokwapua fedha za umma kwa faida yao. Nyaraka zote za wizi
na utoroshaji huu wa fedha na mawasiliano yangu na watu wa Benki ya
NedBank nitayawasilisha mbele ya Kamati ya Bunge ninayopendekeza kuundwa
ili kutazama suala hili.
Mheshimiwa Spika,
Kuna
masuala yanayohusu usalama wa nchi kutokana na kashfa hii ambayo pia
ningependa kuyaonyesha katika Kamati ninayopendekeza kuundwa. Nyaraka
hizo zinaonyesha silaha na aina za silaha zilizonunuliwa na kutoka nchi
gani na kwamba silaha hizo ziliishia wapi. Nimeona kwamba kuyasema
masuala haya waziwazi kunaweza kuhatarisha usalama wa nchi yetu. Hata
hivyo masuala haya ni lazima yafahamike ili hatua stahili ziweze
kuchukuliwa dhidi ya watendaji wa Serikali watakaokutwa na makosa.
Mheshimiwa Spika,
Fedha
zilizoibwa na kutoroshwa kupitia kampuni ya Meremeta na kampuni ya Deep
green ziliishia kwenye akaunti za watu binafsi nje ya nchi. Hata hivyo
mara baada ya kuundwa kwa kampuni ya TanGold, jumla ya dola za
kimarekani milioni kumi ziliwekwa kwenye akaunti ya Kampuni hiyo katika
Benki ya NBC, Corporate Branch. Nambari ya akaunti hiyo pia itatolewa
katika kamati ninayoomba kuunda kwa ajili ya uchunguzi wa kina.
Mheshimiwa Spika,
Mwaka
2004, 2006 na 2007 Tanzania iligawa vitalu vya kutafuta mafuta na Gesi
katika maeneo mbalimbali nchini. Uchunguzi wetu unaonyesha kuwa zaidi ya
dola za kimarekani milioni 56 zililipwa kwenye akaunti za watu binafsi
nchini Switzerland kutoka kwenye kampuni zilizoshinda zabuni ya kutafuta
mafuta na gesi.
Mheshimiwa Spika,
Uchunguzi
nilioufanya kwa msaada wa wachunguzi waliobobea kwenye masuala ya
mifumo ya kifedha ya Kimataifa umeniwezesha kupata nyaraka muhimu
zinazoonyesha watu na namna walivyopata fedha walizoweka katika akaunti
zao nje ya Tanzania.
Mheshimiwa
Spika, mwaka 2004 na 2005 Mwanasiasa wa Afrika Kusini kutoka chama cha
ANC bwana Tokyo Sexwale alitembelea nchini katika ziara ya kibiashara.
Alileta marafiki zake wawili na kuanzisha kampuni iitwayo Ophir Energy
Tanzania limited. Kampuni hii inamiliki vitalu 3 katika pwani ya bahari
ya Hindi blocks 1,3,4. Bwana Tokyo Sexwale alitambulishwa hapa nchini na
raia wa Kongo aitwaye Moto Mabanga. Hivi sasa bwana Moto Mabanga
ameishitaki kampuni ya Ophir Energy kwa kutotimiza masharti
waliyokubaliana kuhusiana na kufanikisha kupatikana kwa vitalu hivyo vya
mafuta. Moto Mabanga ndio alikuwa ‘deal maker’wa kampuni hii na ili
kufanikisha hali hii alihonga sana wanasiasa na maafisa wa Serikali
wanaohusika na ugawaji wa Vitalu vya kutafuta Mafuta na Gesi. Wakati
Ophir wanapewa vitalu hivi sehemu ya hisa za kampuni hii ziligawiwa kwa
baadhi ya watanzania ikionekana kuwa ni hisa kwa ajili ya chama cha CCM.
Hata hivyo uchunguzi wetu unaonyesha kuwa hisa hizo zilikuwa ni za watu
binafsi. Hivi sasa hisa zimeuzwa na fedha kufichwa katika mabenki
mbalimbali nje ya Tanzania. Kuna haja ya kufanya uchunguzi wa kina
kuhusu umiliki wa kampuni ya Ophir Energy wakati wanaingia nchini na
mabadiliko ya umiliki katika kipindi cha miaka minane iliyopita. Vile
vile uchunguzi unapaswa kufanywa kwa vitalu vyote vilivyogawiwa katika
ya mwaka 2003 mpaka 2008 na umiliki wa Watanzania katika makampuni
yaliyopewa vitalu hivyo.
Mheshimiwa Spika,
serikali yetu iagizwe na Bunge lako tukufu kupata taarifa za kina
kupitia njia za kiserikali na njia za wachunguzi binafsi. Mimi kama
Mbunge nilipofikia sasa nahitaji msaada wa Bunge kufanikisha jambo
hili. Nilipofikia sasa ni kutoa taarifa na nyakara zote nilizo nazo na
watu TAASISI zitakazo saidia kwa kamati teule ambayo Bunge litaunda
kushughulikia suala hili mahususi.
Baada ya maelezo hayo, naomba kuwasilisha,
HOJA
BINAFSI YA KABWE ZUBERI ZITTO (MB) KUHUSU KULITAKA BUNGE KUCHUNGUZA NA
KUILEKEZA SERIKALI KUCHUKUA HATUA DHIDI YA RAIA WA WATANZANIA
WALIOFICHA FEDHA NA MALI HARAMU NJE YA NCHI
[Inatolewa chini ya Kanuni ya 54(3)]
Mheshimiwa Spika,
KWA
KUWAkumekuwa na uthibitisho kutoka Mamlaka za nchi ya Switzerland
kwamba kuna raia wa Tanzania wanamiliki fedha za kigeni katika Benki
nchini na kwamba kuna kanuni na taratibu za nchi zinazoendesha na
kuongoza ufunguaji wa akaunti za fedha za kigeni nje ya Tanzania kwa
Watanzania wakazi (residents). Na kwamba kitendo kilichofanywa na
wahusika kuweka mabilioni ya fedha kwenye nchi za nje kinaweza kuwa ni
kinyume na sheria ya “FOREIGN EXCHANGE ACT, 1992”
NA KWA KUWA sheria
hiyo kifungu cha (10) cha Sheria ya Fedha za kigeni kinazuia utoroshaji
wa fedha za kitanzania na isipokuwa kwa kibali cha Gavana wa Benki Kuu
tu, hakuna mtu yeyote atakaye ruhusiwa kusafirisha fedha nje ya
Tanzania. Na kinaeleza kuwa kwa msafiri anayekwenda nje ya nchi
hatoruhusiwa kuondoa na kiasi cha shilingi ambazo zinazidi dola za
kimarekani hamsini. Vile vile kwa mujibu wa Sheria hiyo kifungu cha 6 na
7 na waraka uliotolewa na Gavana wa Benki Kuu kwamba Mtanzania yeyote
mwenye kutaka kufungua akaunti kwenye mabenki nje ya Tanzania lazima
apate kibali cha Gavana.
NA KWA KUWA masharti hayo ya sheria yanaweza kuwa yamekiukwa na wahusika kwa kuhifadhi fedha za kigeni katika mabenki ya nje,
NA KWA KUWA ukiukwaji
huo ni dhahiri kuwa fedha zilizowekwa kwenye mabenki ya nje kwa kiasi
kikubwa ni fedha ambazo hazikupatika kwa njia za halali na kwamba kuna
uwezekano wa ukwepaji mkubwa wa kodi,
NA KWA KUWA,
nchi yetu imekuwa katika matatizo makubwa ya fedha za kigeni, jambo
ambalo limepelekea nchi kushusha thamani ya shilingi ili kukabiliana na
gharama za manunuzi ya bidhaa nje ya nchi,
NA KWA HIYO BASI, ninaliomba Bunge hili liazimie:
Kwamba Bunge lako tukufu liunde Kamati Teule kuchunguza Raia wa Tanzania wenye kumiliki fedha za kigeni na mali nje ya Tanzania. Kamati Teule hiyo ifanye kazi zifuatazo:
Kuchunguza mfumo mzima wa utoroshaji wa fedha na kufichwa nje ya nchi,
kuchunguza na kupembenua mali na fedha haramu dhidi ya halalizinazomilikiwa na raia wa Tanzania katika taasisi za kifedha nje ya Tanzania,
kuchunguza utaratibu mzima wa kugawa vitalu vya utafutaji mafuta na gesi kati ya mwaka 2003 mpaka 2008,
kuchunguza
mtiririko mzima wa utoroshaji wa fedha kutoka Benki Kuu ya Tanzania
kupitia Kampuni ya Meremeta (pia Triannex pty ya Afrika Kusini na Deep
Green Finance ltd) na kupendekeza hatua za kuchukua dhidi ya wahusika
wote wa utoroshaji wa fedha kwenda nje,
kuchunguza
umiliki wa wa watanzania kwenye kampuni zote zenye mikataba ya
utafutaji wa Mafuta na Gesi hapa nchini na namna umiliki huo umekuwa
ukibadilika, mapato (proceeds) zilizotokana na mabadiliko hayo ya
umiliki na kama kodi stahili zimekuwa zikilipwa kutokana na kubadilika
kwa umiliki huo,
kuchunguza
kwa kina mali za Watanzania wote waliowahi kushika nafasi za Uwaziri
Mkuu kati ya mwaka 2003 mpaka 2010, waliowahi kushika nafasi za Uwaziri
wa Nishati na Madini, Uwaziri wa Ulinzi, Ukuu wa Majeshi, Ukatibu Mkuu
wa wizara ya Nishati na Madini, Ukatibu Mkuu wa Wizara ya Ulinzi,
Uanesheria Mkuu wa Serikali, Ukamishna wa Nishati, Ukurugenzi Mkuu wa
TPDC, Uenyekiti na Ujumbe wa Bodi wa TPDC katika ya mwaka 2003 mpaka
2010.
Kwamba
Serikali ilete muswada wa Sheria Bungeni ifikapo Mkutano wa 11 wa Bunge
kwamba itakuwa ni marufuku kwa Kiongozi yeyote wa Umma au mume au mke
wake au watoto wake kuwa na akaunti
katika mabenki nje ya nchi isipokuwa kwa sababu maalumu na kwa kibali
rasmi kutoka kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Kwamba Serikali iwasiliane na Benki ya Dunia ili kupitia Kitengo cha Assets Recovery Unit mabilioni ya Fedha na mali zisizoondoshekazinazomilikiwa na Watanzania katika mabenki ya nchini Switzerland, Dubai, Mauritius na visiwa na maeneo mengine yote ambapo hufichwa fedha na Mali ili kukwepa kodi na kwamba mali hizo na mabilioni hayo yaliyopatikana kiharamu yarudishwe nchini mara moja
Kwamba katika muswada
tajwa hapo juu, Gavana wa Benki Kuu ya Tanzania aimarishiwe mamlaka ya
kutoa kibali kwa Mtanzania yeyote anayetaka kufungua akaunti ya Benki
nje ya nchi na kwamba kila mwaka Gavana atatangaza kwenye Gazeti la
Serikali na magazeti yanayosomwa na wananchi wengi orodha ya Watanzania
walioomba na walioruhusiwa kuwa na akaunti ya Benki nje ya Tanzania.
Kwamba
Watanzania wote wenye akaunti za fedha nje waeleze wamezipataje na
TAKUKURU wachukue hatua za kisheria dhidi ya watu wote wenye kumiliki
fedha na mali kinyume na mapato yao halali.
Kwamba Serikali, katika mkutano wa Bunge wa 11 na
baada ya Taarifa ya Kamati Teule ya Bunge kuhusu Raia wa Tanzania wenye
kumiliki fedha za kigeni kwneye mabenki na mali nje ya Tanzania ilete taarifa ya hatua ilizochukua ili kuziba mianya ya utoroshaji wa fedha nje ya Tanzania.
Kwamba Serikali katika Bajeti ya mwaka 2013/14 itaanzisha
kodi maalumu ‘financial transaction tax’ ya angalau asilimia 0.5 ya
thamani ya ‘transaction’ ili kuweza kuwa na rekodi za uhakika za fedha
ndani na zinazotoka nje ya nchi.
Mheshimiwa Spika,
Naomba kutoa hoja,
…………………….
KABWE ZUBERI ZITTO (MB)
JIMBO LA UCHAGUZI-KIGOMA KASKAZINI