Friday, July 19, 2013

WEMA SEPETU AKAMATWA,SASA YUPO NJIAPANDA YA JELA NA URAIANI,MKASA MZIMA UPO HIVI

KUNA kila dalili kwamba mrembo anayetamba kwenye filamu za Kibongo, Wema Isaac Sepetu ‘Beautiful Onyinye’ au Madam jela inamwit... thumbnail 1 summary


KUNA kila dalili kwamba mrembo anayetamba kwenye filamu za Kibongo, Wema
Isaac Sepetu ‘Beautiful Onyinye’ au Madam jela inamwita na anatakiwa kufanya
maombi ili kukwepa kifungo maishani mwake.


Hali hiyo inafuatia staa huyo kupandishwa kizimbani kwa mara nyingine tena
 Jumatano iliyopita, pale alipopanda katika Mahakama ya Mwanzo ya Kawe
 jijini Dar kwa kosa la kumpiga na kumtukana matusi ya nguoni meneja wa
hoteli moja iliyopo Kawe Beach jijini Dar, Godluck Kayumbu.


Kabla ya  kupandishwa  kwa ‘pilato’,  staa huyo anayemiliki Kampuni ya
Endless Fame alikuwa akisakwa na askari kwa siku kadhaa na kufanikiwa
kuwapiga chenga za hapa na pale.

ANASWA AKIFUTURU
Hata hivyo, mbio zake ziliishia ukingoni Julai 16, mwaka huu, alipokamatwa
saa mbili usiku akiwa anafuturu na wageni wake nyumbani kwake, Kijitonyama
Dar.

MTITI KIDOGO
Askari saba walifika nyumbani kwake wakiwa ndani ya Land Rover ‘difenda’
 kwa ajili ya kumkamata, hata hivyo walipata upinzani kidogo kutoka kwa mlinzi
 wa staa huyo ambaye alikuwa akizuia bosi wake asikamatwe ambapo ilibidi
askari hao wakaze msuli na kutuliza mtiti uliokuwa ukitaka kutokea.

WEMA AGEUKA MBOGO, ALALA SELO
Baada askari kumfikia staa huyo, walimtaka kwenda naye kituo cha polisi kwa
kutumia difenda walilofika nalo ambapo Wema alipinga na kugeuka mbogo
kwa kudai kwamba hawezi kupanda difenda kutokana na hadhi yake.
Pamoja na askari kutaka kumpandisha kwa nguvu, staa huyo alipinga na
 ikakubaliwa apande gari lake aina ya Audi Q7 huku akiwa chini ya ulinzi wa askari.

Safari ikaishia Kituo cha Polisi cha Kawe ambako staa huyo aliandikisha maelezo
 na baada ya zoezi hilo akatupwa selo.

WEMA HAUOZI
Kama lilivyo jina lake, wema hauozi, staa huyo alipata dhamana saa 5 za usiku
 baada ya kudhaminiwa na msanii  mwenzake wa filamu, Kajala Masanja.
Kajala aliwahi kutolewa katika mdomo wa jela na Wema siku za nyuma
baada ya kukutwa na hatia na Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu jijini Dar
alipotakiwa kulipa faini ya shilingi milioni 13 au kwenda jela, Wema alimlipia
kiasi hicho cha fedha.

WAPAMBE FULL SHANGWE
Wapambe wa Wema waliokuwa wamejazana nje ya kituo hicho cha polisi,
walilipuka kwa shangwe baada ya bosi wao kuchomolewa kutoka selo.
Staa huyo aliondoka na gari lake lililokuwa likiendeshwa na meneja wa
kampuni yake aitwaye Petit Man.

ATEMBEZWA KWA MIGUU
Julai 17, asubuhi Wema alirudi kituoni hapo na kuwekwa chini ya ulinzi
kwa ajili ya kupelekwa mahakamani kusomewa mashitaka yake.
Katika hatua ya kushangaza, staa huyo alitembezwa kwa miguu umbali wa
mita 200 kutoka kituo cha polisi hadi Mahakama ya Mwanzo ya Kawe.

APANDISHWA KIZIMBANI
Wema alipandishwa kizimbani na kusomewa mashitaka yake na Mh. Hakimu,
Bernice Ikanda na kudaiwa kufanya vurugu, kushambulia kwa kumpiga
makofi na kumtukana Kayumbu.
Mbele ya hakimu, Wema alikana mashitaka na hakimu aliiahirisha kesi hiyo
mpaka Julai 31, mwaka huu.

IKO SIKU WEMA ATAFUNGWA GEREZANI
Kumbukumbu kutoka kwenye makabrasha yetu zinaonesha kuwa, mrembo
huyo ni mtu wa majanga, mara kwa mara amekuwa akifikishwa polisi na
mahakamani kutokana na ugomvi.

ALIVUNJA KIOO CHA GARI LA KANUMBA
Mwaka 2009, Wema alidakwa na Polisi Kituo cha Magomeni na baadaye
kupandishwa katika Mahakama ya Kinondoni, Dar kwa Hakimu Emilius
Mchalu kwa kosa la kuvunja kioo cha gari la aliyekuwa staa wa filamu za
Kibongo, Marehemu Steven Kanumba chenye thamani ya shilingi milioni
moja. Hata hivyo, Kanumba aliifuta kesi hiyo.

ALIMTISHIA MAISHA BOB JUNIOR
Kama vile haitoshi, mwaka 2011, Wema huyohuyo alikamatwa na Polisi wa
Oysterbay jijini Dar na kufikishwa Mahakama ya Mwanzo, Kinondoni
kwa kosa la kumtusi na kumtishia maisha mwanamuziki wa Bongo Fleva,
Rahem Nanji ‘Bob Junior’.
Katika kesi hiyo, Hakimu Mariam Masamalo alimtia hatiani Wema kwenda
jela miezi sita au kulipa faini ya shilingi 40,000 ambapo alilipa fedha hizo.

ALIMTUSI REHEMA FABIAN
Aidha, mara baada ya Wema kuachiwa huru mahakamani hapo alikamatwa
tena na polisi kwa kile kilichodaiwa kumtusi Miss Kiswahili 2008, Rehema
 Fabian. Wema alipelekwa Kituo cha Polisi cha Oysterbay jijini Dar kwa maelezo
 zaidi.

ALIMTUKANA MSANII
Aidha, Wema amewahi kulala kituo cha Polisi Oysterbay, Dar akiwa na mashoga
 zake, Kajala na Dida kwa madai ya kumshambulia mwigizaji mmoja wa Bongo,
 kwenye pati iliyofanyika Ukumbi wa Bwalo la Polisi, Oysterbay, Dar. Kesi hiyo
 iliisha kwa mazungumzo nje ya polisi.