Wednesday, March 20, 2013

JE UNAZIFAHAMU FAIDA NA HASARA ZA MITANDAO YA KIJAMII

FAIDA NA HASARA ZA MITANDAO YA KIJAMII Ndugu mwana Teknohama, leo naomba tumalizie makala hii ya athari za mitandao ya kijamii katika ma... thumbnail 1 summary

FAIDA NA HASARA ZA MITANDAO YA KIJAMII

Ndugu mwana Teknohama, leo naomba tumalizie makala hii ya athari za mitandao ya kijamii katika maisha ya watu.
Pamoja na mambo yote tulozungumza katika matoleo yalopita, leo ntaongelea kwa kina faida na hasara za mitandao ya kijamii.
Faida za mitandao ya kijamii:
  •  Mitandao ya kijamii inawasaidia watu kutengeneza mahusiano mapya kati ya ndugu na marafiki na pia inaongeza mawasiliano kati ya mtu na mtu na hivyo kuboresha mahusiano
  • Mitandao ya kijamii sasa imefungua mlango mpya kabisa wa chombo kingine cha habari. Imewafanya watu waweze kutuma ujumbe mfupi wa maandishi bure, watu wameza kublogu kama hivi, michezo ya mitandaoni, watu wameweza kubadilishana picha na habari mbalimbali kupitia mitandao hii ya kijamii
  • Mitandao ya kijamii imesaidia kuwaleta watu pamoja wenye mitizamo inayofanana. Mitizamo ya kisiasa, kiuchumi, kiutamaduni, kimapenzi, kimichezo n.k. Watu ambao wamekuwa na matatizo ya kuongea siku hizi wanajisikia raha sana kuwasiliana na watu kupitia mitandao ya kijamii. Imekuwa ni uwanja mzuri wa watu kujionyesha kwa kile alicho nacho moyoni mwake na kukifikisha kwenye jamii
  • Baadhi ya watumiaji wa mitandao hii ya kijamii wamekuwa wakiitumia kutafuta hata kazi, wanafunzi wamekuwa wakiitumia kufanya majadiliano ya kimasomo mitandaoni, wanaharakati wametumia majukwaa ya mitandao ya kijamii kukutana na kuendesha harakati zao mitandaoni. Vyuoni hususai wamekuwa wakiendesha harakati zao kupitia mitandao ya kijamii. Tulishuhudia majuzi tu kwenye mgomo wa madaktari pale ambapo serikali ilipopiga marufuku mikutano ya madaktari, madaktari walibadilisha upepo wa mikutano ya uso kwa uso na kurudi kuwa mikutano ya mitandaoni
  • Baadhi ya watu wameitumia mitandao ya kijamii kupunguza misongo ya mawazo kwa kuwasiliana na watu mbali mbali na kujikuta wamefarijika katika matatizo walonayo. Wataalamu wa saikolojia wanashauri mtu anapokuwa na matatizo ni vema akaishirikisha jamii ili kupunguza mzigo wa kuchukua matatizo peke yake.
  • Mitandao ya kijamii kwa sasa imekuwa ikipanua wigo wake wa mawasiliano kutoka kuwa mitandao ya kijumla  na kuwa bayana zaidi. Kwa mfano watu wamekuwa wakitengeneza makundi ya fani fulani fulani ambapo inawasaidia wataalamu wa fani hiyo kukutana pamoja mtandaoni na hata kuongeza wigo wa kukutana uso kwa uso. Na hii imesaidia watu ambao wamekuwa wanataka kuingiza kwenye makundi ya fani hizo waweze kujumuika nao pamoja

Hasara za mitandao ya kijamii:
  • Mitandao ya kijamii imewafanya watu kutumia muda mwingi kuwasiliana mitandaoni na kuwafanya kuwa  wazembe sana kuwasiliana uso kwa uso.
  • Vijana wengi wanaoibukia kwa sasa hasa wenye umri kuanzia miaka 13 wako kwenye wakati mgumu sana kuathirika na matumizi ya mitandao ya kijamii. Kwanini nasema haya? Vijana wengi hawajui kwamba taarifa mbali mbali wanazoziweka mitandaoni ni taarifa mbazo zinaonekana  hata kama zikifutwa taarifa hizo zinaweza zikapatikana tu. Pamoja na kwamba mpaka sasa hakujawa na uhakika wa taarifa fulani kupatikana baada ya miaka fulani ijayo. Kwa hiyo utoaji mwingi wa taarifa za mtu binafsi inaweza kabisa kumfanya mtu kuwa muhanga wa mapenzi au wizi wa fedha na ujangiri mbali mbali mitandaoni. Watu wanatumia taarifa hizo kufanya uharifu. Kwa hiyo vijana wanatakiwa kuwa makini na taarifa zao wanazoziweka mitandaoni. Hii inaweza kusababisha hata mtu kufukuzwa kazi kama mtu anaweza kutoa taarifa fulani za mwajiri ambazo zinaweza kuleta mkanganyiko kwenye taasisi fulani.
  • Toleo lililopita nilizungumzia jinsi ilivyo ngumu kutambua utambulisho wa mtu. Baadhi ya mitandao ya kijamii imekuwa na desturi ya kuthibitisha utambulisho wa mtu. Kwa mfano, Takwimu zinaonyesha kuwa mtandao wa kijamii wa Facebook umekuwa na watumiaji zaidi ya milioni 700. Lakini nani anaweza kulithibitisha hilo maana kuna mtu unamkuta ana akaunti zaidi ya moja! Wakati mwingine mtu ni mwanaume lakini amefungua akaunti yenye utambulisho wa mwanamke! Hii inaleta mkanganyiko sana kwenye utambulisho wa watumiaji wa mitandao ya kijamii.
  • Muda wa kukutana uso kwa uso kwa ajili ya kubadilishana mawazo na kujichanganya na watu umepungua sana kwa sababu ya ongezeko la watu kutumia muda mwingi sana kwenye mitandao ya kijamii. Wazazi wamekuwa na muda mchache wa kubadilishana mawazo na watoto wao kwa kuwa watoto wao wamekuwa wako bize mitandaoni, wapenzi nao wamekuwa na muda mchache wa kubadilishana mawazo kwa kuwa kila mtu yuko bize kivyake mtandaoni!
  • Utafiti mmoja ulionyesha kwamba theluthi mbili ya wafanyakazi wenye akaunti za facebook huzitumia akaunti zao kubadilishana mawazo na watu mitandaoni kwenye muda wa kazi! Kwa maneno mengine wafanyakazi hawa wanaiba muda wa mwajiri wao! Kuna baadhi ya ofisi hasa za binafsi hapa Tanzania wenyewe wamekuwa wakiondoa mitandao ya kijamii kwenye mitandao ya ofisi zao zinazounganisha wafanyakazi na Intaneti. Changamoto ambayo ofisi hizi inazipata kwa sasa ni ongezeko kubwa la watu kutumia simu za mikononi, pamoja na tablets kuweza kuwasiliana kwenye mitandao ya kijamii kitu ambacho si rahisi kumzuia mtu kuwaisiliana kwenye mitandao ya kijamii. Ofisi za serikali hakika wamekuwa na changamoto kubwa sana kwa wafanyakazi wao wanaotumia mitandao ya kijamii kwani utendaji wao kazi hakika umepungua kwa sababu watu wanatumia muda mwingi sana kwenye mitandao ya kijamii wakati wa kazi.
Hii ndiyo Teknolojia yetu

kama una maoni yoyote juu ya hili naomba unitumie ujumbe wako ktk barua pepe zuberiamiri@gmail.com