KAULI ya Mwenyekiti wa Chama cha Wananchi (CUF), Profesa
Ibrahim Lipumba, kwamba kuna njama za kumwongezea
Rais Jakaya Kikwete, muda wa kuongoza nchi, ni uzushi
mtupu na ni upotoshaji usiokuwa na msingi.
Taarifa ya Kurugenzi ya Mawasiliano ya Ikulu iliyotumwa
kwa vyombo vya habari juzi, ilifafanua kwamba Rais Kikwete
hafahamu kuwepo mipango hiyo, na kumtaka Profesa
Lipumba aisaidie jamii kusema nani anafanya mpango huo,
ili ukweli ujulikane.
“Aidha, Mheshimiwa Rais anawasihi wanasiasa na Watanzania
kwa ujumla, kuacha tabia za uongo na uzushi na kuwapotezea
muda Watanzania kufikiria mambo yasiyokuwepo.
“Ukweli ni kwamba, kama ambavyo amesema mara nyingi,
ni matarajio ya Rais Kikwete kuwa mchakato wa Katiba utakamilika
mwaka 2014, na kuwezesha Uchaguzi Mkuu wa 2015 kufanyika chini
ya Katiba Mpya kama inavyotarajiwa ,” ilieleza taarifa hiyo.
Kwa mujibu wa Ikulu, Rais Kikwete anatarajia baada ya uchaguzi
wa 2015, atapata nafasi ya kustaafu mwisho wa kipindi chake
cha uongozi kwa taifa letu.
|