Miili ya Askari wa Jeshi la Wananchi wa Tanzania JWTZ waliouawa Darfur wiki iliyopita Sajent Shaibu Shehe Othuman wa Mpendae na Koplo Mohamed Juma Ali wa Kwarara imekabidhiwa leo kwa familia zao mara baada ya kuwasili katika Uwanja wa ndege wa kimataifa wa Zanzibar.
Marehemu hao wawili wenye Asili ya Zanzibar ni miongoni mwa Askari saba wa JWTZ waliuawa walipokuwa wakilinda amani chini ya Umoja wa Mataifa na Afrika UNAMID,huko Darfur.
Miili ya marehemu hao imewasili majira ya saa 9 alasiri kwa ndege ya JW 90 34 aina ya Boing ikitokea katika Hospitali ya JWTZ Lugalo Jijini Dar es Salaam.
Mara baada ya kuwasili Uwanjani hapo Miili ya Marehem hao ilipokelewa na Katibu mkuu Afisi ya Makamu wa Pili wa Rais Khalid Mohamed Salum akifuatana na Mwenyeji wake Bregedia Jeneral Kamanda wa Bregedi ya Nyuki Sharif Sheikh Othuman Viongozi wa Vyama na Serikali,Wanafamilia pamoja na Wananchi kwa ujumla.
Aidha huzuni ziliendelea kutanda kwa ndugu na Jamaa waliofika kupokea maiti hizo za Wapiganaji wa Amani ya Dunia chini ya mwenvuli wa UNAMID.
Kwa mujibu wa Taarifa kutoka Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais Shughuli za Mazishi zitafanyika kesho saa nne za asubuhi katika makaburi ya Mwanakwerekwe nje kidogo ya Mji wa Zanzibar.
Aidha shughuli hiyo ya Mazishi itaambatana na taratibu za kijeshi zitakazofanyika Makaburini hapo.
.