
Ronaldo na Bale washerekea ushindi dhidi ya Schalke 04
Mchezaji bora duniani mwaka huu
Cristiano Ronaldo Gareth Bale na Karim Benzima walifunga mabao mawili
kila mmoja na kuisaidia Real Madrid ya uhispania kufuzu kwenye robo
fainali ya kombe la mabingwa barani ulaya baada ya kuinyeshea Schalke 04
ya Ujerumani mabao 6-1 katika mkondo wa kwanza uliosakatwa huko
Ujerumani.
Benzima ndiye aliyefungua kivuno hicho cha mabao baada ya nipe nikupe kunako dakika ya 13.
Mchezaji aliyeigharimu Madrid kitita
kikubwa zaidi msimu huu Gareth Bale akafanya mambo kuwa mawili kwa
nunge dakika saba baadaye .
Kuanzia hapo kampeini ya vigogo hao wa ligi ya uhispania kunyanyua taji lao la kumi barani Uropa ilikuwa mbioni
kufuzu kwa hatua ya robo fainali .
Ronaldo alimpangua Joel Matip kwa miondoko ya
aina yake na kufunga la tatu akimwacha kipa wa Schalke Fahrmann asijue
azibe wapi azue wapi.
Masaibu ya wenyeji hao yaliongezeka Karim Benzema alipofuma bao la nne .
Bale akaongezea bao la tano kisha nyota wa Ureno
Ronaldo akafunga kiziba mkonga na kudidimiza kabisa mtumaini ya timu ya
tatu ya Ujerumani baada ya mabingwa Bayern Munich na washindi wa pili
Borussia Dortmund kusonga mbele katika hatua ya robo fainali ya mchuano
huo msimu huu.
Uchungu uliwazidi mashabiki wa nyumbani na
wachache waliosalia uwanjani walishuhudia bao la kukata na shoka la
nyota wao Klaas-Jan Huntelaar .
Huntelaar aliyeichezea Madrid (2009) kwa mkopo alifuma mkwaju wa kipekee uliomwacha Iker Casillas ameduwaa.
Hata
hivyo bao hilo la kufutia machozi la dakika ya mwisho ya mechi
haitakuwa na faida mbali na kunusuru hadhi ya kocha Jens Keller Schalke
itakapozuru bernabou baada ya majuma mawili kwa mkondo wa pili.

Fernando Torres asherekea bao lake
Katika mechi nyengine iliyosakatwa usiku wa jana
huko Instabul,Uturuki ,matumaini ya pekee ya timu ya Uingereza kusonga
mbele katika hatua ya robo fainali yalitegemea matokeo baina ya wenyeji
Galatasaray na Chelsea .
Matokeo ya mkondo wa Kwanza
- Barcelona 2-0 Man City
- Paris St-Germain 4-0 Bayer Leverkusen
- Atletico Madrid 1-0 AC Milan
- Bayern Munich 2-0 Arsenal
- Manchester United 0-2 Olympiakos
- Borussia Dortmund 4-2 Zenit St Petersburg
- Chelsea 1-1 Galatasaray
- Real Madrid 6-1 Schalke
Kwa kila hali na mizani mechi hii ilitarajiwa
kuwa ngumu kwa Galatasaray chini ya kocha wa zamani wa Manchester city
Roberto Mancini ikiongozwa na aliyekuwa mshambulizi wa Chelsea Didier
Drogba na Emmanuel Ebue zamani akiichezea Arsenal ilikuwa inakabiliana
na The Blues chini ya Kocha Jose Mourinho .
Uwanjani mashabiki wa nyumbani walinyamazishwa na bao la dakika ya 9 ya kipindi cha kwanza iliyofungwa na Fernando Torres.
Roberto Mancini alilazimika kufanya badiliko la mapema ilikuzia kuabishwa na wimbi la mashabulizi ya vijana wa Mourinho .
Katika kipindi cha pili juhudi za Galatasaray
kujinasua zilizaa matunda Aurelien Chedjou alifunga bao la kusawazisha
baada ya kutumia vyema mpira wa kona uliomchanganya Peter Cech .
Bao hilo ndilo litakaloamua mshindi baina ya
timu hizo mbili zitakapokutana katika mechi ya mkondo wa pili tarehe 18
mwezi Machi huko Stamford Bridge .