Rais John Magufuli.
Wakizungumza na Nipashe kwa nyakati tofaut jana, walisema hatua
hiyo imeonyesha jinsi Rais Magufuli alivyo na uwezo wa kufanya maamuzi
kulingana na umuhimu wa jambo katika wakati husika kwa manufaa ya wengi.
Mkazi wa Tabata, wilayani Ilala, Joel Mrutu, alisema hatua hiyo
kiutendaji ni jambo zuri kwani ameonyesha kukerwa na matumizi mabaya ya
fedha za serikali.
“Hatua aliyoichukua kiutendaji ni jambo zuri kwani Rais ameonyesha anakerwa na matumizi mabaya ya fedha serikali,” alisema.
Alisema, Dk. Magufuli akiendelea na msimamo huo inawezekana ikapatikana Tanzania mpya wanayoitaka wananchi.
Mkazi wa Temeke, Ali Jabir, alisema Rais Magufuli ameonyesha mfano
wa kuigwa kwa kujali maisha ya watu kwa kusisitiza fedha za umma
kutumika kwenye masuala ya msingi.
Kwa upande wake, Bwana Afya wa Manispaa ya Kinondoni, Dk. Mathias
Kapiza, alisema kitendo alichokifanya Dk. Magufuli kitasaidia kuwaamsha
kuhusu madhara na ukumbwa wa ugonjwa wa kipindupindu ulioyakumba maeneo
mengi nchini na kushirikiana na serikali kupambana nao.
“Mabadiliko ya kweli yameanza kuonekana kwa kufuta siku ya Uhuru na
kuifanya kuwa siku ya usafi, hii itawasaidia wananchi kutambua jukumu
la kupambana na maradhi na kuchukua hatua kuutokomeza,” alisema Dk.
Kapiza.
Naye Mhadhiri wa Kikuu cha Tumaini, tawi la Dar es Salaam
(Tudarco), Danford Kitwana, alisema kinachoendelea kufanywa na Rais
Magufuli ni namna ya kubana matumizi mabaya ya fedha za serikali na
kupongeza siku hiyo kutumika kufanya usafi.
Alimtaka kuangalia sherehe nyingine ambazo hazina umuhimu wa
kutumia fedha nyingi ili fedha hizo zielekezwa kwenye mambo yenye tija
kitaifa. Kaimu Mwenyekiti wa Chama cha Wafanyakazi wa Reli Kanda ya Dar
es Salaam, Yasin Mleke, alisema anaunga mkono hatua hiyo kwani hali ya
uchumi ni mbaya huku serikali ikiwa ina mambo mengi ya kufanya ikiwamo
malipo ya mishahara ya watumishi, madeni ya wafanyakazi, uboreshaji wa
huduma za afya na elimu.
Naye Msemaji wa Jumuiya za Taasisi za Kiislamu Tanzania ambaye pia
ni Katibu wa jumuiya hiyo, Sheikh Rajab Katimba, alisema hadhani kama ni
sahihi kufuta sherehe hizo kwa kigezo cha kuifanya siku ya usafi ndiyo
nchi nzima itakuwa safi.
Alisema kufanya hivyo kunapoteza historia ya nchi na kutaka suala
la usafi kuwekewa mikatati na Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii.
Aliyekuwa Mgombea ubunge Jimbo la Segerea, Julius Mtatiro, alisema
yeye haamini katika matamko badala yake vitu vinavyofanyika kisheria na
siyo mtu kufanya kwa ajili ya utawala wake.
Alisema sherehe za Uhuru zinatakiwa kuwapo kila mkoa pasipokuwapo
mambo mengi yatayogharimu fedha, ikiwamo kurusha ndege za kivita hewani,
magwaride na maonyesho ya makomando na posho.
Mtatiro alisema huenda hatua hiyo imefanyika kutokana Hazina
kuishiwa fedha, akidai kuwa nchi nyingi za Afrika vyama tawala hutumia
fedha za serikali kwenye uchaguzi.
Ijumaa iliyopita Rais Magufuli alizuia matumizi y Sh. milioni 265
zilizokusudiwa kutumiwa na Ofisi ya Bunge kwa ajili ya hafla ya wabunge
kupongezana baada ya uzinduzi rasmi wa Bunge la 11, mjini Dodoma.
Aliamuru zitumike Sh. milioni 15 tu na fedha nyingine zilizobaki
zitumiwe kununua vitanda kwa wagonjwa wanaolala chini katika Hospitali
ya Taifa ya Muhimbili (MNH).
Aidha, Jumatatu iliyopita aliagiza kufutwa kwa sherehe za Uhuru na kutaka siku hiyo itumike kufanya usafi nchi nzima.
CHANZO:
NIPASHE