
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk. John Magufuli.
Kadhalika, inaelezwa kuwa Dk. Magufuli aliyeahidi kuleta mabadiliko
ya kweli wakati akiomba kura kwa Watanzania kabla ya kuibuka na ushindi
wa asilimia 58.46 dhidi ya wapinzani wake katika uchaguzi mkuu Oktoba
25, sasa yuko mbioni kutangaza baraza lake la mawaziri litakalokuwa na
wizara 15, idadi inayofanana kwa kiasi kikubwa na ile ya Baraza la
Mawaziri la miaka ya 1980 lililoundwa na Rais wa Awamu ya Kwanza, Baba
wa Taifa hayati Mwalimu Julius Nyerere. Serikali ya awamu ya nne ya Rais
Jakaya Kikwete, ilimaliza muda wake Novemba 5, 2015 ikiwa na Wizara
30. Kadhalika, alipoingia kwa mara ya kwanza mwaka 2005, Rais Kikwete
alikuwa na serikali kubwa yenye mawaziri na naibu wao zaidi ya 60.
Kufikia leo, Rais Magufuli aliyeapishwa Novemba 5, mwaka 2015,
tayari ameshamteua Mbunge wa Ruangwa, Kassim Majaliwa, kuwa Waziri Mkuu
wa serikali yake ya awamu ya tano na Ijumaa iliyopita alizindua rasmi
Bunge la 11.
Chanzo kimoja cha uhakika kimeiambia Nipashe jana kuwa hivi sasa,
tayari Rais Magufuli kwa kushirikiana na wasaidizi wake, ameshakamilisha
sehemu kubwa ya mchakato wa kuunda baraza lake la mawaziri na kwamba,
kinachosubiriwa sasa ni kulitangaza wakati wowote kuanzia sasa.
Chanzo hicho kiliambia Nipashe kuwa Dk. Magufuli ambaye
amejichimbia mjini Dodoma tangu mwishoni mwa wiki iliyopita, anatarajiwa
kutangaza baraza lake dogo la mawaziri wakati wowote kuanzia leo.
“Halitakuwa sawa na hili alilomaliza nalo Rais Kikwete… na wala
halitakuwa na watu wengi kama lile aliloingia nalo kwa mara ya kwanza
Rais Kikwete mwaka 2005. Ni baraza dogo tu na wizara kadhaa
hazitakuwapo,” chanzo kiliiambia Nipashe.
Kwa mujibu wa ibara ya 55 (1) ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania,
mawaziri wanakuwa wajumbe wa Baraza la Mawaziri na pia kwa mujibu wa
ibara ya 54, mawaziri huteuliwa na rais baada ya kushauriana na Waziri
Mkuu.
“Kuna mambo madogo bado hayajakamilika… baada ya hapo Mheshimiwa
Rais atalitangaza Baraza la Mawaziri siku yoyote kuanzia leo. Kimsingi
mkakati wake ni kuwa na baraza dogo lenye wizara 15,” kilieleza chanzo
hicho.
Aidha, ilielezwa zaidi kuwa sura kadhaa katika baraza hilo dogo
zitakuwa mpya na kwamba, mawaziri waliokuwamo katika serikali ya awamu
ya nne wana nafasi ndogo ya kuteuliwa katika baraza hilo.
“Kwa kiasi fulani Baraza hili jipya linafanana na lile la Serikali
ya Mwalimu Nyerere miaka ya 1980… lina wizara chache sana, zenye lengo
la kubana matumizi ya serikali lakini likiwa na uhakika wa kuchapa kazi
usiku na mchana ili kutimiza lengo la Rais Magufuli katika kuwaletea
maisha bora Watanzania,” chanzo kiliongeza.
BARAZA LA MAWAZIRI LA NYERERE
Uchunguzi wa Nipashe kupitia vyanzo mbalimbali ikiwa ni pamoja na
maandiko mbalimbali, umebaini kuwa iwapo Magufuli ataunda Baraza lake
kwa kuangalia muundo wa Mwalimu Nyerere miaka ya 1980, maana yake baadhi
ya wizara maarufu hazitakuwapo tena kwani zitakuwa miongoni mwa zile 15
zitakazofutwa na majukumu yake kuhamishiwa katika wizara nyingine za
idadi kama hiyo zitakazosalimika.
Kumbukumbu zinaonyesha kuwa miaka ya 1980, Mwalimu Nyerere alikuwa
na serikali yenye wizara 15; ambazo ni Wizara ya Elimu; Wizara ya
Mipango; Wizara ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa; Wizara ya Mambo ya
Ndani; Wizara ya Ujenzi; Wizara ya Mawasiliano na Uchukuzi na Wizara ya
Kazi na Ustawi wa Jamii.
WQizara nyingine wakati huo ni Wizara ya Habari na Utamaduni;
Wizara ya Afya; Wizara ya Nishati, Madini na Maji; Wizara ya Sheria;
Wizara ya Viwanda na Biashara; Wizara ya Kilimo na Wizara ya Fedha.
KASI YA MAGUFULI
Wakati Watanzania wakiendelea kusubiri kwa hamu kusikia baraza la
mawaziri la Rais Magufuli, inaelezwa kuwa baadhi ya wabunge kutoka Chama
Cha Mapinduzi (CCM) wako njiapanda kuhusiana na majina ya wateule
watakaokuwamo katika kuunda serikali.
Inaelezwa kuwa, kama ilivyokuwa katika uteuzi wa jina la Waziri
Mkuu, hivi sasa kuna usiri mkubwa pia kuhusiana na majina ya wateule wa
Rais Magufuli kwa nafasi hizo za uwaziri.
“Tofauti na ilivyokuwa katika mika michache ya hivi karibuni,
uteuzi huu wa mawaziri umebaki kuwa wa siri sana na hadi sasa hakuna
majina ya uhakika ya watu wanaotazamiwa kuwamo kwenye Baraza la Rais
Magufuli, “ mmoja wa wabunge aliiambia Nipashe jana.
Ilielezwa zaidi kuwa mbali na kuwapo kwa usiri mkubwa, pia staili
ya utendaji kazi aliyoanza nayo Rais Magufuli imekuwa ikiwatisha baadhi
ya wabunge wa CCM waliokuwa na matumaini ya kuteuliwa kuwa mawaziri.
“Misimamo ya Rais Magufuli haitoi matumaini ya ulaji kwa wateule wa
nafasi hizo… wengine wameshaanza kuingiwa hofu kwamba hata wakiteuliwa,
hakuna maslahi makubwa binafsi watakayoyapata zaidi ya kutakiwa
wajiandae kutumikia wananchi kwa moyo mmoja na tena kwa kujituma
kwelikweli, chini ya Magufuli uwaziri siyo kazi rahisi ya kuikimbilia,”
mbunge mwingine aliongeza.
Katika hotuba yake Ijumaa wakati akizindua Bunge, Rais Magufuli
alianisha mambo kadhaa aliyosema yamekuwa kero kubwa kwa wananchi na
hivyo serikali yake itafanya kazi kubwa ya kuyashughulikia, baadhi ya
maeneo hayo yakiwa ni ya kuboresha elimu ambayo itatolewa bure hadi
kidato cha nne, kuinua mapato na pia kupambana na kukomesha vitendo vya
rushwa na ufisadi.
Kadhalika, hivi karibuni Rais Magufuli ametangaza hatua kadhaa za
serikali yake kubana matumizi na badala yake kuelekeza fedha katika
shughuli za maendeleo; baadhi ya hatua hizo zikiwa ni kupiga marufuku
safari holela za viongozi kwenda nje ya nchi, kufuta sherehe siku ya
uhuru na badala yake kuamuru siku hiyo iwe ya kufanya usafi ili
kukabiliana na kipindupindu na pia aliamuru zaidi ya Sh. milioni 200
zilizochangwa kwa ajili ya wabunge kupongezana baada ya kuapishwa wiki
iliyopita zielekezwe katika Hospitali ya Muhimbili ambako zilisaidia
kununuliwa kwa vitanda vya wagonjwa 300.
“Tusubiri tu kusikia baraza lake la mawaziri limewajumuisha kina
nani. Lakini ukweli unabaki palepale kwamba uwaziri siyo kazi lelemama
kwa serikali hii. Maana Rais (Magufuli) kaweka wazi kuwa mtu (Waziri)
yeyote akiboronga, anamfuta kazi mara moja… kinachotakiwa ni kazi tu,
hakuna kwenda Ulaya ovyo, wala hakuna tafrija na makongamano yenye nia
ya kuhalalisha ulaji kwa vigogo,” chanzo kiliongeza.
CHANZO:
NIPASHE
No comments
Post a Comment